MASOMO YA MISA, MACHI 24, 2022: ALHAMISI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA
Updated at: 2024-05-27 07:09:44 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kw amashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.
Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Unirudishie furaha ya wokovu wako.
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:29 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Paulo aliwaambia wakuu wa kanisa ya Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Au: Aleluya.
Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu
Wafalme watakuletea hedaya. (K)
Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu; (K)
Enzi yake i juu ya Israeli;
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)
Aleluya, aleluya,
Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya.
Siku ile, Yesu alisali akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.
Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.
Updated at: 2024-05-27 07:09:47 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani.
Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.
Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.
Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.
Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.
Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu utumwani. (K)
Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.
Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.
Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake.
Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:50 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Alikuja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.
1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K)
Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
2. Macho ya watu yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. (K)
3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Aleluya Aleluya!
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya
Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.
Neno la Bwana..... Sifa Kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:46 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena likuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Sahmu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalame wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.
Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamni kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.
Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sana kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.
Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema. Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia nawe utakuwa safi. Lakini Naaman akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.
Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakisema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; naye nyama ya wmili wak eikarudi ikawa kama nyam aya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.
Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu.
Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. (K)
Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)
Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
Na hata maskani yako. (K)
Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu. (K)
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.
Yesu alifika Nazareti akawaambia makutano hekaluni: Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na weny eukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakazwa ila Naamani, mtu wa Shamu.
Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipiita katikati yao, akaenda zake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:24 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Waisraeli walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya: Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)
Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
Wapendwa, hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake veye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, am have kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
Aleluya, aleluya, Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Yesu alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza
magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:41 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Wasiomsadikia Mungu walisema hivi, huku wakimfikiri yasiyo kweli, Zaidi ya hayo na tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Asema ya kwamba anamjua Mungu, na kujiita mtumishi wa Bwana. Ametuwia magombezi ya fikira zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu; maan amaisha yake si sawasawa na masiha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni. Tuanhesabiwa naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Wenye haki asema kuwa mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yake.
Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.
Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo.
Uso wa Bwan ani juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwan akasikia,
Akawaponya na taabu zao zoe. (K)
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)
Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja.
Bwana huzikombo a nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)
Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na mnyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.
Baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuw awakitafuta kumwua.
Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye laipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.
Basi baadhi ya watu wa yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu tuna jua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.
Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.
Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:23 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo. nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.
Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana;
Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji
Katika mikono ya watu watendao maovu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Kwa ajili yako nimestahimili laumu,
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu yao wanaokulaumu zimenipata. (K)
Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana,
Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu,
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. (K)
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yetu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu
Bahari na vyote viendavyo ndani yake. (K)
Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia uli mwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, alive mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, ee Bwana,
Ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.
Yesu aliwaambia mitume wake: Msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum, Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:47 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi, siku zako zitakapo timia, ukalala na Baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake.
Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
Wazao wake watadumu milele.
Fadhili za Bwana nitaziimba milele;Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)
Nimefanya agano na mteule wangu,Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.Wazao wako nitawafanya imara milele,Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)
Yeye ataniita, Wewe baba yangu,Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)
Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa Imani. Kwa hiyo ilitoka katika Imani, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa Imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ilia pate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Heri wakaao nyumbani mwako, Ee Bwana.
Updated at: 2024-05-27 07:09:38 (2 years ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema, Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote.
Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.
Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.
Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema, Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote wawili.
Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati aya bonde la uvuli wa mauti
Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe change kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zinanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Yesu aliwaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.
Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi nay eye aliyenipeleka. Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.
Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui kama mngalinijijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.
Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.