Njia za kupima Afya
Njia mbalimbali hutumika kupima hali ya lishe, njia hizi ni;
1. Vipimo vya umbile la mwili
2. Vipimo vya maabara
3. Kuchukua historia ya ulaji na maradhi
Vipimo vya umbile la mwili
Baadhi ya vipimo ambavyo vinaweza kutumika kutoa tahadhari kuhusu magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ni;
1. Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).
2. Mzunguko wa kiuno.
3. Uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga.
4. Kulinganisha uzito na umri.
Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).
Hiki ni kipimo kinachotumika kuangalia uwiano wa urefu na uzito wa mtu, ni muhimu kuchukua vipimo kwa usahihi.Uwiano wa uzito katika Kilogramu na urefu katika mita hupatikana kwa kutumia kanuni ifuatayo:
BMI= uzito (Kg)/Urefu2 (m2)
BMI huwa na viwango mbalimbali vilivyowekwa na shirika la Afya duniani (WHO) kutafsiri hali ya lishe ya mtu ambavyo ni
1. BMI chini ya 18.5 = uzito pungufu.
2. BMI kati ya 18.5 mpaka 24.9= uzito unaofaa.
3. BMI kati ya 25.0 mpaka 29.9 = unene uliozidi.
4. BMI ya 30 au zaidi = unene uliokithiri au kiribatumbo.
Mahitaji ya chakula mwilini hutegemea umri, jinsi, hali ya kifiziolojia (kama ujauzito na kunyonyesha), hali ya kiafya, kazi na mtindo wa maisha. Uzito wa mwili hutegemea na chakula unachokula, pamoja na shughuli unazofanya, mara nyingi unene hutokana na kula chakula kwa wingi.
Unene uliokithiri unachangia kwa kiwango kikubwa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu, na saratani. Uzito uliozidi unapaswa kupunguzwa ili kuepuka magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza
No comments yet. Be the first to share your thoughts!