Neno Albino linamaanisha mtu mweupe, linatokana na neno la lugha ya Kilatini - albus-linamaanisha “eupe”. Kuanzia karne ya 17 neno Albino limekuwa likitumika katika kueleza hali ya kundi la viumbe hai (watu, wanyama na hata mimea) ambao wana upungufu au ukosefu wa rangi katika ngozi, macho na nywele. Kwa binadamu ni bora kutumia maneno “Watu wanaoishi na ualbino kwani itamaanisha kuwa ni watu kama wengine ila wanaishi na hali tofauti ya “ualbino”. Katika kitabu hiki maneno haya mawili yatatumika. Lugha inajenga dhana na kuunda hali ya ukweli / uhalisi. Kwa sababu hiyo ni lazima tuache kutumia maneno kama “zeruzeru”. Neno hili linamaanisha sifuri mara mbili au mtu asiye na thamani. Utumiaji wa neno hili ni dharau ya utu na kulaumu watu wanaoishi na ualbino kama kosa lao.