Misa Takatifu ina sehemu kuu ngapi?

Misa Takatifu ina sehemu kuu mbili
1. Litrujia ya Neno
2. Liturujia ya Ekaristi

Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu ngapi?

Litrujia ya Ekaristi ina sehemu kuu tatu
1. Matayarisho ya vipaji
2. Sala ya Ekaristi
3. Ibada ya Komunyo

Liturujia ni nini?

Liturujia ni tendo la Kristo mwenyewe na Kanisa la kumtukuza na kumwabudu Mungu Baba; na hivyo kutekeleza fumbo la Wokovu kwa kuwatakasa watu

Liturujia ina nafasi gani katika Kanisa?

Liturujia ambayo ni tendo takatifu kuliko yote ndiyo chemichemi ambayo nguvu ya uhai wa Kanisa inabubujika na Kristo anaendeleza Kazi ya Ukombozi wetu

Katika liturujia waamini wanafanya nini?

Katika Liturujia waamini wanashiriki kwa matendo na kwa Ibada adhimisho lote yaani sala, nyimbo na matendo yote ya Ibada; na asiposhiriki matendo hayo kikamilifu, anakosa mafao kamili ya neema ipatikanayo katika Ibada hiyo.

Kilele cha Liturujia ni nini?

Kilele cha liturujia ni Sadaka Takatifu ya Misa

Kwa namna gani Mungu Baba ndiye asili na lengo la Liturujia?

Mungu Baba ndiye asili na lengo la Liturujia kwa sababu katika liturujia anatujaza Baraka zake katika Mwanae Yesu Kristo, naye anatumiminia Roho Mtakatifu mioyoni mwetu

Katika Liturujia Roho Mtakatifu anatenda nini kuhusiana na Kanisa?

Katika Liturujia Roho Mtakatifu analiandaa Kanisa likutane na Bwana wake

Ni nani hupanga Taratibu za Liturujia?

Mama Kanisa ndiye mwenye kupanga taratibu zote za Liturujia Katika mwaka mzima.
Huu mpango huitwa mwaka wa kanisa

Katika mwaka wa kanisa tunakumbuka nini?

Katika Mwaka wa Kanisa tunakumbuka natunaadhimisha matukio na mafumbo yote ya ukombozi wetu na hivyo twapata neema zake

Adhimisho la Liturujia Hutumia Ishara na Alama zipi?

Adhimisho la Liturujia Hutumia Ishara na Alama zinazohusiana na uumbaji, maisha ya binadamu na historia ya wokovu; nazo ni;
  1. mwanga,
  2. maji,
  3. moto,
  4. kuosha mikono/kupaka mafuta
  5. kumega mkate,
  6. kuwekea mikono n.k

Nani huadhimisha Liturujia?

Liturujia iliyo kazi ya Kristo Kuhani Mkuu na kichwa cha Kanisa huadhimishwa na kusanyiko lote, kila mmoja kulingana na kazi yake.

Liturujia inaadhimishwa wapi?

Liturujia inaadhimishwa pale waamini walipokusanyika kwa lengo hilo; kwa sababu Ibada katika Roho na Kweli ya Agano Jipya haifungwi na mahali fulani tuu, kwani dunia yote ni Takatifu

Liturujia Ifanyike mahali pa namna gani?

Liturujia ifanyike mahali palipoandaliwa vizuri iwezekanavyo kwa kuwa katika tendo la Ibada tunakutana na Mungu

Mwaka wa Kanisa una vipindi vikubwa vingapi?

Mwaka wa Kanisa una vipindi vikubwa vitano ambavyo ni;
1. Majilio = Majuma manne
2. Noeli = Kuzaliwa hadi Epifania
3. Kwaresma = Majuma sita na Juma Kuu
4. Pasaka = Siku ya Pasaka hadi Pentekoste
5. Kipindi cha mwaka majuma 34

Majilio ni nini?

Majilio ni kipindi cha Dominika nne cha kujiandaa na Sherehe ya Kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani NOELI.
Kinawakilisha karne zote za Agano la Kale

Kwaresma ni nini?

Kwaresma ni kipindi cha siku 40 cha kujiandaa kuadhimisha Sherehe kuu ya PASAKA yaani kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Tunajiandaa kwa Kufunga Kusali, Kutubu, na Matendo Mema.

Wakati wa kwaresma yawapasa waamini kufanya nini?

Waamini wanapaswa kujitakasa zaidi kwa;
  1. kusali,
  2. kufunga,
  3. toba na
  4. matendo mema

Kipindi cha Pasaka hudumu kwa siku ngapi?

Kipindi cha Pasaka hudumu kwa siku 50;
Yaani kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Sherehe ya Pentekoste

Siku za Dominika Kanisa huadhimisha nini?

Kila Dominika Kanisa Huadhimisha kumbukumbu ya Fumbo la Pasaka; Yaani;
Mateso, Kifo na Ufufuko wa wa Bwana, katika hali ya kutomwagika damu tena.

Kwa nini Jumapili inapaswa kuitwa siku ya Bwana au Dominika?

Jumapili inapaswa kuitwa Siku ya Bwana au Dominika kwa sababu ndiyo siku Bwana amefufuka Mshindi wa Dhambi na Mauti

Kipindi cha Mwaka ni nini?

Kipindi cha Mwaka ni kipindi cha kufurahi kuishi matunda ya ukombozi wetu

Sikukuu Kubwa Kupita zote Katika Kanisa ni ipi?

Sikukuu Kubwa Kupita zote Katika Kanisa ni PASAKA