Biblia inashuhudia kuwa watu wanatofautiana
Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na jinsi walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa ajili ya taifa lake.
Abrahamu alimuamini Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate baraka ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18).
Yosefu, mwana mpenzi wa Yakobo, alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20).
Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka [[utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, âWala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musaâ (Kumb 34:10-12).
Waliofuata ni Yoshua, Debora, Gideoni, Ruthu, Samweli, wafalme Daudi na Solomoni, manabii Eliya, Isaya, Yeremia, Ezekieli na wengineo.
Mwishoni Yesu Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, âNi mkuu kati ya uzao wa wanawakeâ (Lk 7:24-28).
Elizabeti, mama wa Yohane, alijiona hastahili kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu, akamuita, âMama wa Bwana wanguâ (Lk 1:43).
Bikira Maria si mtu wa ziada katika mpango wa Mungu bali ni mshiriki mkuu wa ukombozi wa binadamu. Maria amechangia wokovu kwa kukubali mpango wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae, amlee na kumfuata kiaminifu hadi msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa mmoja tu: âTazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosemaâ (Lk 1:38).
Tukichunguza nafasi yake katika fumbo hilo, tunaweza kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49), kwa kuwa, âMtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Munguâ (Yoh 3:27).
Yale yote ambayo Wakristo wengi wanayasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu huku akiitikia kwa hiari fumbo la mpango wake.
Utabiri kuhusu Bikira Maria kwenye Biblia
Biblia inatupatia utabiri uliotolewa na Mungu mwanzoni mwa historia kuhusu mwanamke atakayemshinda nyoka wa kale (Shetani): âNitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chakoâ (Mwa 3:15). Juu ya [[Eva wa kale, ambaye alidanganywa na kuangushwa na Shetani atende dhambi, imesemwa: âAdamu akamwita mkewe jina lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio haiâ (Mwa 3:20). Hata hivyo Adamu na Eva wa kale wametuletea kifo (Rom 5:12). Mababu wa Kanisa wanamtazama Bikira Maria kama Eva mpya aliyemshinda Ibilisi na kuwa mama wa wote walio hai. Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Mama yake awe Mama wa waliokombolewa kwa kumkabidhi mwanafunzi, tena yule aliyempenda zaidi. âPenye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Kleopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, âMama, tazama, mwanaoâ. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, âTazama, mama yakoâ. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. (Yoh 19:26-27).
Utabiri mwingine ulisema, âTazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli, yaani Mungu pamoja nasiâ (Isa 7:14). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:34-35, âMariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Munguâ. âImba, ee binti Sion, piga kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu katikati yakoâ (Sef 3:14-15). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:28: âMalaika akaingia nyumbani mwake akamwambia, âFurahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu pamoja naweââ. âUmebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu mileleâ (Yudithi 14:7; 15:9). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:42, âAkapaza sauti kwa nguvu akasema, âUmebarikiwa wewe kuliko wanawake wote, na yeye utakayemzaa amebarikiwaââ.
Bikira Maria ni fumbo la ajabu alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Jamaa yake Elizabeti alimpongeza tena akiongozwa na Roho Mtakatifu, âHeri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwanaâ (Lk 1:45).
Hivyo manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua Maria kwa heshima. Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yalitimia katika Agano Jipya: ukombozi ulianza Bikira Maria alipokubali kwa imani fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu. Bikira Maria hakuwa âchomboâ tu kilichotumika bila ya kuelewa, bali alikuwa mshiriki huru wa kazi ya ukombozi ya Mwanae, kwa kuwa alipopashwa habari na malaika alikubali kwa hiari mpango wa Mungu akisema, âMimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonenaâ (Lk 1:38).
Bikira Maria katika maisha ya Yesu
Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii wazee wake: âBasi, akarudi pamoja nao Nazareti, akawa anawatiiâ (Lk 2:51).
Ishara ya kwanza kwenye maisha ya hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na huruma kwa wenye shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi wake wakamwamini. Yohane alisimulia hivi, âSiku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, âHawana divaiâ. Yesu akamwambia, âMama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadiaâ. Mamaye akawaambia watumishi, âLo lote atakalowaambia, fanyeniâ. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, âJalizeni mabalasi majiâ. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, âSasa tekeni, mkampelekee mkuu wa mezaâ. Wakapelekea. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maj), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, âKila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasaâ. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yoh 2:1-12).
Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya roho kuliko ya mwili. âBasi, mtu mmoja akamwambia, âMama yako na ndugu zako wako nje, wataka kusema naweâ. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo, âMama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?â Kisha akanyosha mkono wake juu ya wanafunzi wake akasema, âHawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu na dada yangu na mama yanguââ (Math 12:46-50). Vilevile, wakati wa utume wake, alimsikia âmwanamke mmoja katika lile kundi la watu akisema, âHongera kwa mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyeshaâ. Yesu akamjibu, âBarabara, lakini heri yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na kulishikaââ (Mk 11:27-28).
Bikira Maria alivyoshiriki Mateso ya Yesu
Katika kumfuata Mwanae Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni uchungu kama upanga utakaopenya moyo wake, âTazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama upanga utauchoma moyo wakoâ (Lk 2:34-35).
Bikira Maria alishiriki kwanza mateso ya ukimbizi huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiuawe na Herode Mkuu, âHivyo Yosefu aliamka akamchukua mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka Herode alipokufaâ (Math 2:14-15).
Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua kuteswa kwa Yesu; wanafunzi walipokimbia au kumtazama kwa mbali, yeye alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata Mwanae. Kutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, alipoyashuhudia yote aliteseka sana katika moyo wake safi, kiasi kwamba Bernardo wa Klervoo akasema, âMsalaba wa Yesu uliwasulubisha wote wawili, Yesu mwilini na Mama yake moyoniâ. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.
Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, âNa sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristoâ (Kol 1:24). â⌠maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wakeâ (Rom 8:17b).
Pale msalabani Bikira Maria, kwa njia ya mtume Yohane alifanywa Mama wa wote wanaompenda Mwanae; kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana ameshindwa.
Bikira Maria baada ya kifo cha Yesu
Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, akilivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa sala yake. âHao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria Mama yake Yesu na ndugu zakeâ (Mdo 1:14).
Yesu alisema, âNinayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli woteâ (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa kadiri ya utabiri wake kuwa ataheshimiwa na vizazi vyote, âKwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye heriâ (Lk 1:48).