Watu wanokunywa kupitia kiasi huathiri jamii kwa njia mbalimbali. Madhara mengine hutokea kwa kuwa wanafanya vitu ambavyo wasingevifanya iwapo wasingekuwa wamelewa. Watu wakilewa, huweza kuwa na hasira, wagomvi hivyo basi huwadhuru wengi kiakili na kimwili. Isitoshe, ajali nyingi za kazini na barabarani hutokea watu wakiwa wamelewa. Mara nyingi watu wasiokuwa na hatia na vilema hupoteza maisha yao kutokana na ajali zinazohusiana na ulevi. Watu wanaokunywa pombe kupita kiasi hupunguza uangalifu na hivyo basi kuchangia katika kuenea kwa VVU kwenye jamii. Watu wanaokunywa pombe wanaweza pia kufanya ujambazi katika jamii. Pia wanaokunywa kupita kiasi si wafanyakazi wa kutegemewa kwani hutumia muda mwingi nje ya sehemu zao za kazi. Watu waliozoea kunywa pombe nyingi hupoteza pesa zao nyingi kununua pombe na muda wao mwingi kufikiria jinsi ya kupata pesa za kunywea pombe. Kutokana na gharama za kununua pombe familia zao hukosa pesa za vitu muhimu kama kodi ya nyumba, ada na sare za shule na chakula. Vijana wanaokunywa pombe huanza kuiba pesa nyumbani kwao ili kununulia pombe. Matumizi mabaya ya pombe mara nyingi husababisha matatizo au kuvunjika kwa familia, au urafiki. Vilevile husababisha matokeo mabaya shuleni au kuacha kabisa shule, hali ambayo inaweza kusababisha kukosa nafasi za kazi, kujitegemea wewe mwenyewe na kusaidia famila yako na jamii.