Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)
Hii ni aina ya mizinga inayotumika sana na wengi. Gharama yake ni ndogo kiasi kulinganisha na mingine. Ni aina nzuri sana kwa mtu anaeanza ufugaji wa nyuki kwa kuwa ni wa gharama nafuu. Mfugaji wa nyuki anaweza kutengeneza mzinga Yya aina hii mwenyewe kama ana utaalamu wa useremala.
Faida ya Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)
• Ni rahisi kukagua asali iliyo tayari.
• Ni rahisi kuvuna asali kuliko kuvuna toka kwenye mzinga wa kienyeji.
• Ni rahisi kuwatunza nyuki wakati wa kiangazi na inapokuwa hakuna maua. Kwa mfano unaweza kuwapatia nyuki chakula ili kuongeza uzalishaji wa asali.
• Ni rahisi kurina asali ukilinganisha na mizinga ya magogo inayotundikwa juu ya mti, kwa kuwa haihitaji vifaa maalumu.
• Aina hii ya mizinga huwekwa kwa kuninginia jambo ambalo siyo rahisi kushambuliwa na wadudu/wanyama wanaokula asali kwa kuwa Inajaa haraka sana wakati ambao ni msimu wa asali kutengenezwa kwa wingi.
Hasara ya Mizinga ya Kifuniko juu (Top bar)
• Kichane kwenye mzinga wa boksi hakina kishikizo hivyo huvunjika kwa urahisi sana kama hakitashikwa kwa uangalifu.
• Masega huvunwa pamoja na asali, kwa hiyo nyuki wanalazimika kutengeneza tena masega mengine ambapo husababisha kupungua kwa uzalishaji wa asali.
Mzinga wa Langstroth
Mzinga wa Langstroth unaweza kukupatia asali zaidi kulinganishwa na mizinga mingine Hii ni aina nzuri na rahisa sana ya mzinga. Mizinga hii hufahamika kama mzinga wa fremu, kwa kuwa ina fremu ambazo vichane vya masega hujishikiza. Chumba kikubwa ambacho malkia hutagia mayai. Malkia anazuiliwa kuhama kwenda chumba kingine kwa kutumia waya. Kwenye chemba maalumu ya kutagia juu yake pana chemba ya kuhifadhia asali.
Vichane vya masega vinatengezwa kwenye fremu na si kwenye nguzo kama ilivyo kwenye Top bar. Ili kuvuna asali, mfugaji akiwa na masega yaliyojaa asali, hutumia vifaa maalum kwa ajili ya urinaji na kuhifadhi asali bila kupata tabu.
Mzinga wa Langstroth ni gharama kiasi kulinganisha na mizinga mingine.Unaweza kuipata kutoka katika taasisi zinazojiusisha na uuzaji wa mizinga, taasisi na karakana binafsi, au wakala wa Serikali.